Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema limefanikiwa kuwakamata majambazi watano wanaodaiwa kuhusika na tukio la uvamizi katika kituo cha polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga jijini Dar es salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema majambazi hayo yamekamatwa Mbagala jijini Dar es salaam ambapo katika tukio hilo wamekamata pia fedha kiasi cha shilingi milioni 170 na bunduki 16 ambapo 14 kati ya hizo ni zile zilizoibiwa katika kituo cha Stakishari.
Aidha, Kamanda Kova ameongeza kuwa bado wanawatafuta watu kadhaa wanaotuhumiwa ni wafuasi wa genge hilo hatari la uhalifu ambalo mbali na kuua polisi wanne na raia watatu katika kituo cha Stakishari, genge hilo pia linahusika na uporaji fedha katika taasisi mbalimbali za fedha nchini.
Kova ametoa wito kwa wananchi na wana habari kuendelea kusaidia jeshi hilo katika utoaji wa taarifa zonazohusu matukio ya uhalifu ili kukomesha vitendo hivyo.