Jumapili , 1st Mar , 2015

Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameahidi kuigawa wilaya ya Chunya ili kupata wilaya mbili kabla ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Uamuzi wa waziri mkuu kuigawa wilaya ya Chunya haraka unatokana na maombi ya wananchi wa jimbo la Songwe hususan katika kijiji cha Buyuni ambao wameamua kulala chini kwenye mavumbi, huku mbunge wa jimbo la Songwe, Mheshimiwa Philip Mulugo akipiga magoti chini na kumwomba waziri mkuu kuigawa wilaya hiyo kwa madai kuwa ina maeneo makubwa kijiografia hali ambayo inakwamisha maendeleo ya wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya akamweleza waziri mkuu kuwa ukubwa wa wilaya ya Chunya ni asilimia 46 ya ardhi yote ya mkoa wa Mbeya hivyo maombi ya wananchi hao yana hoja ya msingi, huku Mkuu wa wilaya ya chunya Deodatus Kinawiro akielezea uwezo wa halmashauri ya wialaya ya Chunya kiuchumi kuwa inajitegemea kwa asilimia 15.

Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda amesema kuwa kikwazo pekee cha kuigawa wilaya hiyo ni idadi ndogo ya watu, lakini kutokana na hali ambayo ameiona analazimika kuigawa wilaya hiyo haraka, jambo ambalo ameahidi kulifanya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.