Jumatatu , 2nd Nov , 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezindua Chama cha Kuendeleza Ufugaji Nyuki Tanzania (Tanzania Beekeeping Development Organization – TABEDO) na kukitaka kishirikiane na makampuni binafsi ili kuendeleza sekta hiyo kwa haraka.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitundika mzinga wa nyuki wakati alipotembelea kikundi cha hifadhi ya misitu na ufugaji nyuki cha Kambi ya Nduta.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao walishiriki uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma.

TABEDO kinaundwa na wafugaji nyuki, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki, watengenezaji na wasambazaji wa vifaa vya ufugaji nyuki.

Waziri Mkuu amesema taarifa za wachambuzi wa biashara ya mazao ya nyuki kimataifa zinaonyesha kuwa soko la asali ulimwenguni linategemea kuongezeka hadi kufikia tani millioni 1.9 zenye thamani ya Dola za Kimarekani billioni 12 kwa mwaka huu.

Alisema soko la Jumuiya ya Nchi za Ulaya linaongezeka kwa asilimia 2.5 kila mwaka. Na kwamba jambo hilo limetokana na viwango vya uelewa wa faida za matumizi ya mazao ya nyuki na kutambua umuhimu wake katika kuboresha afya kwa walaji au watumiaji.

Pinda ameongeza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa mazao ya nyuki yana bei nzuri ndani na nje ya nchi hivyo kinachotakiwa ni kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki kwa kuzitumia taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Global Standard 1 (GS1).