Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Waziri mkuu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mizengo Pinda amewaagiza wakurugenzi na wakuu wa mikoa kuhakikisha sheria na kanuni za mfuko wa fedha za barabara zinafuatwa hasa kupitia ripoti ya kila robo mwaka ya matumizi ya mifuko wa barabara na kijiridhisha.
Mh. Pinda ameongeza kuwa ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha ni lazima ripoti za kila robo mwaka za mapato na matumizi ziweze kuwasilishwa ili kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa barabara za halmashauri.
Waziri Pinda ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa mfuko wa barabara Jijini Arusha unaowakutanisha wadau wa barabara wa mwaka ambapo amewakumbusha wasimamizi wa mfuko huo kuepuka rushwa kwani huchangia kujengwa kwa barabara zisizokidhi viwango.
Wakati huo huo, Idara ya uhamiaji mkoa wa Njombe inawashikilia wahamiaji haramu 21 raia wa Ethiopia walioingia nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na EATV, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Njombe, Rose Mhagama amesema wahamiaji haramu hao walikamatwa katika Halmashauri ya Mji wa Makambako wakiwa ndani ya roli la simenti lililokuwa likendeshwa na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Nyange.
Amesema baada ya wahamiaji hao kuwahoji wamebaini kuwa kuna watu watatu wanaofanyabiashara ya kusafirisha wahamiaji haramu, ambao mmoja yuko Kenya, mwingine Mkoani Mbeya kwa upande wa Tanzania na mmoja nchini Malawi.