Jumatano , 21st Sep , 2022

Zaidi ya wasichana laki moja wanatarajiwa kufikiwa na mfumo wa kidigitali unaofahamika kama Panda digital sms  ambapo utawawezesha wasichana wa Tanzania kuweza kuendesha biashara kidigitali sambamba na kuunganishwa na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani na nje ya Tanzania

Hatua ambayo inatokana na kubainika kwamba kuna pengo kubwa katika matumizi ya kidigitali kati ya msichana na mvulana hasa wanaoishi maeneo ya vijijini

Mkurugenzi wa shirika la Her Initiative Lidya Charles Moyo  akizungumza na waandishi wa habari  leo amesema  wamebaini pia kwamba wasichana wengi wa vijijini hawana simu janja , hawana internet na hata ule ujuzi wa awali wa kuweza kutumia majukwaa hayo ya kidigitali hivyo kupitia mfumo huo ambao ni bure utawasaidia kupata elimu na taarifa za kujiendeleza kwa kujua namna gani unaweza kuongeza soko la biashara yako na  pili ni vitu gani unaweza kuviandaa Ili uwe na biashara yenye mafanikio zaidi

Naye mbunifu wa mifumo ya teknolojia kutoka shirika hilo Giveni Edward amesema Kwa uzoefu uliokuwepo mifumo mingi ya jumbe fupi yaani sms lazima ulipie lakini kwa mfumo huo ni tofauti kwani hata kama hauna salio kwenye simu yako unaweza kutuma na kupokea ujumbe wenye kukuelekeza unachopaswa kufanya kwenye biashara yako lakini ni lazima uwe umejisajili kwenye mfumo huo

Naye meneja mahusiano na mawasiliano Bi Lucy Moto amewasihi wasichana kujiunga na mifumo hiyo ya kidigitali ambayo vijana wengi wamekuwa wakiitumia kama fursa za kujiajiri tofauti na wasichana huku akisisitiza kwamba teknolojia imekuwa ikikua kila siku na ikitumika vizuri italeta mageuzi makubwa ya kiuchumi na biashara kwa wasichana