
Pakistan imefunga mpaka wake dhidi ya Afghanistan siku ya leo Jumapili, Oktoba 12,2025 kufuatia majibizano ya risasi kati ya vikosi vya nchi hizo mbili usiku kucha katika mashambulizi ambayo Kabul imedai kuwaua wanajeshi 58 wa Pakistan.
Wanajeshi wa Afghanistan walifyatua risasi kwenye vituo vya mpakani vya Pakistan jana Jumamosi jioni, huku wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ikisema kuwa hii ilikuwa ni kulipiza kisasi mashambulizi ya anga ya Pakistani nchini Afghanistan mapema wiki hii. Pakistan ilisema kuwa ilijibu kwa mashambulio ya bunduki na mizinga.
Afghanistan ilisema katika taarifa kuwa imewaua wanajeshi 58 wa Pakistani, lakini haikutoa maelezo kuhusu jinsi ilivyojua kuhusu majeruhi. Pia ilisema kuwa wanajeshi 20 wa Afghanistan waliuawa au kujeruhiwa.
Hakukuwa na jibu la haraka kutoka Pakistan. Maafisa wa usalama wa Pakistan wamesema wamesababisha maafa kwa jeshi la Afghanistan lakini hawakutoa idadi ya wale waliowauwa.
Mataifa yote mawili yamedai kuharibu nguzo za mpaka za upande mwingine. Maafisa wa usalama wa Pakistan wamechapisha picha za video, ambazo walisema zilionyesha namna Afghanistan ilivyopigwa.
Mabadilishano ya ufyatulianaji risasi yalimalizika mapema asubuhi ya leo Jumapili lakini katika eneo la Kurram nchini Pakistan, milio ya risasi imeendelea, kulingana na maafisa wa eneo hilo na wakazi. Kabul imesema kwamba imesitisha mashambulizi kwa ombi la Qatar na Saudi Arabia.
Islamabad inautuhumu utawala wa Taliban kwa kuwahifadhi wanamgambo wanaoshambulia Pakistan, mashtaka ambayo Kabul inakanusha. Vivuko viwili vikuu vya mpaka vya Pakistan na Afghanistan, huko Torkham na Chaman, vimefungwa sanjari na vivuko vitatu vidogo, huko Kharlachi, Angoor Adda na Ghulam Khan, pia vilifungwa, maafisa wa eneo hilo walisema.