mmoja wa majeruhi katika tukio la mauaji Kilosa
Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro limeanza kufanya oparesheni ya kuwatafuta watuhumiwa waliohusika na mauaji ya watu watatu wakiwemo wakulima wawili na mfugaji mmoja, kufuatia mapigano yaliyozuka kati ya wakulima na wafugaji katika bonde la matembele linalounganisha kijiji cha Mabwegere na Mbigiri wilayani kilosa mkoani Morogoro.
Mkuu wa wilaya ya Kilosa Elis Tarimo akizungumzia tukio hilo wakati alipotembelea majeruhi katika hospitali ya mission St Joseph Dumila amesema mauaji hayo hayatavumilika na jeshi la polisi litahakikisha linawakamata waliohusika na tukio hilo.
Tarimo amewataja waliofariki dunia kuwa ni Joseph Peter (26) mkulima, Rajabu Selemani (55) mkulima na Kaduru Kashu (30) mfugaji na wengine wamelazwa hospitalini hapo huku mmoja akihamishiwa katika hospital ya mkoa wa Morogoro.
Kufuatia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ametupia lawama Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchelewa kuleta wasuluhishi wa mgogoro huo kama serikali ilivyoahidi kwa lengo la kuhakiki upya mipaka ya vijiji ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, iliyodumu kwa muda mrefu.
Nao majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Mission Joseph Dumila wamelalamikia serikali kushindwa kumaliza tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo wameelezea mapigano yalivyo tokea nae muuguzi wa zamu Melania Shayo amesema wakulima wawili walifariki dunia wakati wakipatiwa matibu na kukiri kupokea maiti moja ya mfugaji aliyeuwawa wakati wa mapigano hayo.
Mapigano haya yamekuja siku chache baada ya nyumba 41 kuchomwa moto zikiwemo za wakulima na wafugaji kufutia mgogoro wa ardhi katika kijiji cha mabwegere wilayani kilosa, ambapo mkuu wa wilaya aliwakutanisha wakulima na wafugaji kwa lengo la kumaliza mgogoro huo lakini hata hivyo mkutano huo uligubigwa na mivutano na wafugaji kuondoka kabla ya mkutano kumalizika..