Rais Barack Obama amemaliza ziara yake ya siku tatu nchini Kenya kwa kutoa hotuba yake ya mwisho katika uwanja wa michezo wa Kasarani ambapo amekemea utamaduni wa kuwakandamiza wanawake na kutowapatia fursa za elimu na uchumi.
Akiongea mara baada ya kukaribishwa na dada yake Dk. Ouma Obama mbele ya wananchi wa Kenya wapatao 5,000, Rais Obama amesema utamaduni wa kuwafanya wanawake kuwa kama raia wa daraja la pili ni mbaya na unairudisha nchi nyuma.
Ameeleza kuwa uzoefu unaonesha kuwa jamii inayotoa usawa wa elimu kwa watoto wa kike na wa kiume imekuwa na amani na maendeleo ya haraka na huo ndio ukweli kwa Marekani na pia ni ukweli kwa jamii ya wananchi wa Kenya.
Pamoja na mambo mengine rais Obama amekemea rushwa na kuhimiza viongozi kuhakikisha kuwa kunakuwa na sheria kali za kudhibiti rushwa na wananchi wa kawaida waseme rushwa sasa basi ni wakati wa maendeleo.
Aidha, rais Obama amesema kuwa anaamini hakuna kinachoweza kumzuia kijana wa Kenya kufanikiwa katika jambo lolote na kuahidi kuwa serikali ya Marekani itawaunga mkono na kuwasaidia vijana ili wafanikiwe kiuchumi huku vijana wakiwa na maoni tofauti.