Sehemu ya nyavu haramu zikiteketezwa kwa moto
Serikali kupitia idara ya uvuvi mkoani mara imeendesha oparesheni kali na kufanikiwa kukamata zana haramu ambazo zilikuwa zikitumika kuvulia samaki katika ziwa Victoria zenye thamani ya zaidi ya milioni Tisini kisha kuziteketeza kwa moto.
Akizungumza wakati wa kuteketeza zana hizo haramu za uvuvi katika zoezi ambalo limefanyika nje kidogo ya mji wa musoma, kaimu afisa mfawidhi doria na udhibiti wa uvuvi kanda ya mara Bw Alli Mzee Said, amesema jumla ya zana haramu 11,397 zimekamatwa katika opareshini hiyo.
Amesema katika oparesheni hiyo ambayo imedumu kwa siku 21 na kuhusisha wilaya za Rorya, Butiama na Bunda, jumla ya makokoro ya dagaa na samaki aina ya sangara 155 na kamba zake za kuvulia kokoro mita 39,205 zimekamatwa pamoja na nyavu 11,242 ambazo haziruhusiwi kisheria kuvulia samaki pia zimekamatwa.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa wilaya ya musoma Bw John Henjewele, akizungumza baada ya kuwasha moto kwa ajili ya kuteketeza zana hizo haramu, amesema serikali haina nia ya kuwafilisi wavuvi na wafanyabiashara wa nyavu, bali wanapaswa kuzingatia sheria na kwamba zoezi hilo linakuwa endelevu katika kupambana na uvuvi haramu katika ziwa Victoria.
Nao baadhi ya wakazi wa mkoa wa mara Bw David Katikiro na Bw Emmanuel Bwimbo, pamoja na kuipongeza serikali kwa jinsi inavyopambana na uvuvi haramu katika ziwa Victoria, lakini pia wamesema kuna haja kwa serikali kuchukua hatua ya kudhibiti uingizaji wa zana hizo kutoka nje ya nchi, hatua ambayo wamesema itasaidia kupambana na uvuvi huo haramu