Jumanne , 16th Feb , 2016

Chama cha NRA kimesema kitashiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar na kukanusha taarifa zilizotolewa awali na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho kuwa chama hicho hakitashiriki uchaguzi huo.

Chama cha siasa cha NRA cha nchini Tanzania kimeviomba vyama vya siasa nchini kushiriki uchaguzi wa Zanzibar uliopangwa kufanyika March 20 mwaka huu mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kutokana na dosari zilizojitokeza.

Wakizungumza jijini Dar es salaam leo viongozi wa chama hicho wanasema wapo tayari kushiriki uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache zimepita baada ya mgombea urais wa chama hicho visiwani Zanzibar kutangaza kujitoa kugombea pamoja na kujitoa kwa chama hicho.

Viongozi hao wamekanusha vikali kujitoa katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa ni uchaguzi pekee utakaoweza kuwaingiza viongozi wa nchi madarakani.