Jumanne , 27th Nov , 2018

Ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya msaada wa kisheria, imeelezwa kuwa moja ya matatizo yanayoongoza kwenye vituo vya kutoa msaada wa kisheria bure ni migogoro ya ndoa.

Picha ya ishara ya ndoa

Hayo yamebainishwa leo na Wakili kutoka chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) George Mollel, kupitia MJADALA wa East Africa Television ambapo ameeleza kuwa kupitia wiki hii huwa wanabaini makundi mengi yana uhitaji wa msaada wa kisheria.

''Watu wana uhitaji mkubwa sana na hapa ndipo unagundua kuwa kuna makundi mawili ambayo malalamiko mengi ni ya Kijinai na ya madai ambayo ndio mengi ikiwemo migogoro ya ndoa, ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi'', amesema Wakili.

Aidha amefafanua kuwa kuanzia Novemba 25 mpaka 30, huwa kuna nafasi ya kipekee kwa kila mtu mwenye uhitaji wa msaada wa kisheria jambo ambalo hufanyika bure kabisa kutoka kwa wanasheria na mawakili.

Pia ameeleza kuwa sheria ya msaada wa kisheria ambayo iliundwa mwaka 2017 na ikasaidia kuwatambua wasaidizi wa kisheria ambao hutoa msaada wa kisheria katika ngazi ya chini kabisa ikiwemo vijijini jambo ambalo limekuwa na matokeo chanya katika kutoa msaada kwa watu wa vijijini na kumalizai migogoro yao.