Jumanne , 22nd Jul , 2014

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanane kwa kuhusika na tukio la kutupa mabaki ya miili ya binadamu katika msitu mdogo uliopo eneo la Mpiji, Kata ya Mbweni, Wilaya ya Kinondoni.

Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna Suleima Kova.

Akiongea leo Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova, amesema miongoni mwa watu waliokamatwa ni pamoja na madaktari wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), ambapo miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwa ajili ya mafunzo.

Kamanda Kova amesema kuwa jeshi la polisi limeunda jopo la watu saba la maafisa wa upelelezi linaloongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jafari Mohamed ili kubaini sababu zilizopelekea Chuo cha IMTU kutupa viungo hivyo vya Binadamu katika maeneo hayo.

Aidha, Kamanda Kova amesema jeshi la polisi pia litawahusisha Mkemia Mkuu wa Serikali na Mwanasheria Mkuu ili kubaini miili hiyo ni ya kina nani, ilipatikana wapi, kwa kibali gani ikiwa ni pamoja na kufahamu hatua za kisheria zitakazotumika kuwaadhibu wahusika.