Jumamosi , 4th Mar , 2017

Mbunge wa Bunda mjini, Esther Bulaya amewataka wabunge wenzake kujitoa kwa nafasi walizonazo ili kuwasaidia mabinti wenye uhitaji wa taulo za hedhi (Pedi), kuepuka kukosa kuhudhuria darasani kwa siku zisizopungua 60 kwa mwaka.

Ester Bulaya alipowasilisha mchango wake katika ofisi za EATV

Akiwa amewasilisha mchango wake katika ofisi za East Africa Limited katika siku ambayo anakumbuka siku yake ya kuzaliwa (tarehe 3, Machi) Bulaya amesema kwamba kampeni ya Namthamini imemfanya awafikirie mabinti wengi kutoka jimboni kwake na taifa kwa ujumla jinsi wanavyopata wakati mgumu baada ya kushindwa kupata vifaa ya kujisitiri waingiapo kwenye mzunguko wa hedhi.

Ilikuwa ni kumbukumbu siku ya kuzaliwa ya Ester Bulaya

"Leo nikiwa natimiza miaka 37  kuelekea siku ya mwanamke duniani kampeni hii imenifanya nijisikie kama mama na mwanamke kamili, kwa kuwa siku hii inanihusu moja kwa moja,kampeni hii imenigusa sana na niwaombe wabunge wote bila kujali jinsia wala chama kwa sababu kama wewe ni mwanaume jua una wapiga kura mabinti, tujitoe sana katika kampeni hii kuwasaidia mabinti na wadogo zetu" - alisema Bulaya

Hata hivyo Bulaya ameahidi kuwasilisha ombi lake kwa  serikali katika mkutano ujao wa bunge juu ya kushiriki kikamilifu katika kumtengenezea mwanafunzi wa kike mazingira rafiki ya kuweza kujisitiri pindi wanapokuwa katika hedhi.

 

Mbunge Viti Maalum - Lathifa Chande

"Tukiwa bungeni tutaiambia serikali ipunguze kodi ya bidhaa zinazohusu wanawake moja kwa moja kama hizi taulo za hedhi (Pedi) ili kuwaokoa mabinti wengi wanaoshindwa kuhudhuria masomo wakianza mzunguko wa hedhi".- Bulaya

Bulaya amekabidhi taulo za hedhi ambazo hakutaja thamani yake akiwa ameongozana na Mbunge wa viti Maalumu Lindi, Lathifa Chande pamoja na pesa taslimu shilingi laki moja kutoka kwa Mbunge wa Kawe, Mh. Halima Mdee na kuahidi kabla ya kufikia tarehe ya kilele  ataongeza vifaa hivyo kwa kadri atakavyojaaliwa.