Jumapili , 4th Aug , 2024

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Deus Sangu amepiga marufuku walengwa wa mfuko wa maendeleo ya jamii  (TASAF) wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 65, wenye ulemavu, akina mama wajawazito pamoja  na

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kwela, Deus Sangu

na watoto kufanya kazi za kujitolea huku akionya watendaji watakaozembea kusimamia suala hilo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao

Mhe. Sangu  ametoa kauli hiyo leo  kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi  wa Kata ya Lusaka  kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika  kwenye  vijiji vya Lowe, Lusaka, Kizumbi na Kamnyazya  vilivyopo Jimbo la Kwela , Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
 
Amezitaja kazi hizo za kujitolea ambazo huratibiwa na TASAF kuwa ni ulimaji wa barabara pamoja na uchimbuaji wa mitaro ya barabara

Amesema kundi hilo lisisumbuliwe kufanya kazi hizo kwani sio sawa kutokana na hali zao. 

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amezitaka kaya zinazonufaika na mpango wa TASAF kuhakikisha kama zina wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na wanatarajia kujiunga chuo kikuu wawasilishe majina yao katika ofisi za  Halmashauri zao ili waweze kupata kipaumbele cha kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu utakaowawezesha kuendelea na masomo ya chuo kikuu kwani bodi hiyo imeingia mkataba na TASAF.

Amesema lengo la TASAF kuingia mkataba na Bodi ya Mikopo wa Elimu ya Juu ni kuhakikisha  watoto wanaotoka katika kaya maskini hawakosi mkopo ili kuhakikisha  wanafaulu  ili badae waweze kurudi kwa ajili ya kuzikomboa Kaya zao kwenye lindi la umaskini.