Johnson Minja (Kushoto) akiwa mahakamani (Dodoma)
Akitoa taarifa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Dodoma, Rebecca Mbilu, Mwendesha mashtaka wa serikali Rose Shio amesema kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo umeshakamilika na kuiomba mahakama kutengua dhamana ya mshtakiwa kutokana na kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.
Amesema kuwa pamoja na hilo Mwenyekiti huyo amekuwa akiendelea kufanya mikutano na wafanyabiashara kwa ajili ya kuwahamasisha wasiendelee kulipa kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki za efds kitenda alichosema kuwa ni kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.
Hata hivyo wakili wa mshtakiwa, Godfrey Wasonga ameiambia mahakama kuwa tangu mteja wake apewe dhamana ahajawahi kuitisha mikutano na wafanyabiashara kwani hata juzi hakuwa na mkutano bali wafanyabiashara waliokuja mjini Dodoma kusikiliza kesi ya mwenyekiti huyo, waliposikia kuwa yupo Dodoma walikwenda kumsalimia baada ya kupata taarifa kuwa yuko katika hoteli ya Image Hill.
Na kuhusu suala la kufunga maduka mwenyekiti huyo hakuwashawishi wafanyabiashara nchini kufunga maduka yao bali ni wafanyabishara wenyewe ndo walioamua kufunga maduka yao kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi ya mwenyekiti wao.
Hata hivyo hakimu Mbilu amesema kuwa ameridhika na hoja za upande wa mashtaka na hivyo akatengua dhamana ya Minja na kumtaka kubaki rumande hadi April Mosi mwaka huu ambapo kesi yake itatajwa tena.
Amesema kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa maelezo ya awali April 9 mwaka huu kutokana na ushahidi wa kesi hiyo kukamilika.