Jumanne , 2nd Dec , 2014

Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa mbili katika jiji la Mwanza leo Asubuhi imesababisha athari mbalimbali za kijamii na kiuchumi yakiwemo mafuriko makubwa, uharibifu wa mali na miundombinu.

Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa mbili katika jiji la Mwanza leo Asubuhi imesababisha athari mbalimbali za kijamii na kiuchumi yakiwemo mafuriko makubwa, uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na baadhi ya watu kukosa mahali pa kuishi huku familia moja yenye watoto watano wanaoishi mabatini mtaa wa Mwembegiza wakiokolewa na askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji baada ya kusombwa na maji.

Mvua hiyo imeanza kunyesha majira ya saa Moja asubuhi na kusababisha mafuriko ambayo yalikuwa yakisomba kila kitu, yakiwemo magari matatu na samani mbalimbali za ndani huku watu wazima 18 ambao walikuwa wamefikia kwenye nyumba za kulala wageni na kwenye makazi yao halikadhalika wamekijikuta wakiwa hawana la kufanya baada ya maji kujaa pomoni ndani ya nyumba hizo.

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wameishauri serikali kuwaondoa watu waliojenga pembezoni mwa mkondo wa mto Mirongo unaoanzia mto Simiyu kufuatia eneo la Mabatini kukumbwa na mafuriko kila mara, huku mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo Nyamhanga Kimore Marwa mkazi wa mabatini mwembegiza akisimulia mkasa uliomfika wa kupotelewa na watoto wake watano.

EATV pia imeshuhudia vibao vya alama za barabarani viking’olewa na mafuriko hayo, magari madogo ya abiria jijini Mwanza maarufu kama Hiace, yakikwama na kusababisha foleni kubwa kwenye daraja la Mwananchi, baadhi ya magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye gereji jirani na kambi ya jeshi la polisi yakizingirwa na maji huku pia mapipa ya kuhifadhia mafuta yakisombwa na mafuriko katika daraja la mtaa wa Misheni.