Alhamisi , 5th Mar , 2020

Katika kusherehekea mafanikio ya mwanamke, East Africa Television na East Africa Radio inaendelea na kampeni ya #MwanamkeKinara ambapo wanawake mbalimbali wanapata fursa ya kueleza jitihada zao zilizopelekea kufaninikiwa ili kuwasaidia wengine.

Doris Mollel (wa pili kutoka kulia) akiwa na watangazaji wa Dadaz

Leo Machi 5, 2020, kupitia kipindi cha DADAZ mrembo ambaye amewahi kushiriki a kushinda mashindano mbalimbali ya urembo nchini Doris Mollel ameeleza namna ambavyo amekuwa akishiriki kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa Njiti.

'Nina miaka 29, nilizaliwa kabla ya wakati 'Njiti' na tulikuwa mapacha na mwenzangu David. Kilichonisukuma kuanzisha #DorisMollelFoundation ni changamoto wanazopitia watoto waliozaliwa 'Njiti' hususani kukosekana kwa mashine za kuwasaidia kupumua' - Doris Mollel.

Aidha Doris ameongeza kuwa, 'Niliwahi kutembelea Hospitali nikakutana na daktari akanionesha jinsi watoto waliozaliwa kabla ya muda wanavyohangaika, baada ya hapo nikaamua kuisaidia serikali kwa kufanikisha uwepo wa mashine za kutosha katika hospitali zetu'.

Pia amesisitiza kuwa, 'Nitoe angalizo, watoto wengi wanaozaliwa 'Njiti' sababu kubwa ni mimba za utotoni na mikoa kama Dodoma na kanda ya ziwa zimeathirika kwa kiasi kikubwa, pia jamii inawatunza watu wanaowapa mimba watoto wadogo'.

Amesema kupitia Doris Mollel Foundation ambayo aliianzisha mwaka 2015, wanatoa elimu kwa jamii haswa wavulana maana wao ndio huwashawishi mabinti kuingia kwenye mahusiano hivyo kama wao wakipata elimu ni rahisi kuthibiti mimba za utotoni ambazo husababisha kujifungua watoto 'Njiti'.