Mvua zilizonyesha kwa muda mfupi katika jiji la Dar es Salaam zimesababisha mafuriko katika maeneo ya katikati ya jiji na kusababisha baadhi ya maduka kufungwa na magari kuzimika barabarani kutokana na kuingiwa na maji kulikotokana na tatizo sugu la miundombunu ya maji taka.
EATV imetembelea katika maeneo mbalimbali ya jiji hapo katika makutano ya barabara ya Morogoro na Bibi titi imeshuhudiwa idadi kubwa ya maduka kufungwa kutokana na hofu ya kuingiliwa na maji yaliyokuwa yamefurika barabarani ambapo baadhi ya madereva wakilazimika kusukuma magari yao baada ya kuziba kutokana na kuingia maji huku watembea kwa wakilazika kupita kwenye maji hali inayoweza kuhatarisha afya zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameitaka serikali kutenga fedha na kuweka mikakati maalumu ili kuondoa kero sugu ya tatizo la miundombinu ya maji taka katika jiji la Dar es Salaam.
Wakazi hao wamelalamikia serikali kushindwa kuweka miundombinu imara ambayo itaweza kuzuia tatizo la mafuriko yanayotokea pindi mvua zinaponyesha na kuwataka baadhi ya viongozi kuingia mikataba yenye tija kwa jamii husika.
Kwa upande wao wakazi wa Magomeni mtaa wa Chalinze wamemtaka mkuu wa mkoa kutekeleza ahadi yake yakujenga mifereji ambayo itasambaza maji kwenda baharini na kuondoa tatizo la kutuama maji mbele ya nyumba zao na kuhatarisha afya za jamii husika.
Aidha EATV imepita katika eneo la Jangwani na kukuta eneo maalumu ya ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo haraka likiwa limezungukwa maji ambapo baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo hayo wameitahadharisha serikali kuwa mradi huo hautaweza kufanya kazi kama inavyokusudiwa hususani wakati wa mvua bila kuongeza kina cha daraja la mto msimbazi ili kuwezesha maji mengi kuelekea baharini.
Wakati huo huo Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), leo imetoa tahadhari kwa wakazi wa Kusini na mikoa ya Pwani kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huku ikiwataka watumiaji wa bahari kuwa makini kwa wakati huu.
Akizungumza na East Africa Radio Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Dk. Agnes Kijazi amesema mvua hizo zitanyesha mfululizo mpaka mwishoni mwa mwezi wa kwanza mwakani na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na mgandamizo wa hewa katika visiwa vya Madagascar