Jumatano , 24th Dec , 2014

Zaidi ya nyumba 51 zinazokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 200 katika manispaa ya Singida zimebomolewa na mapaa yake kuezuliwa na mvua kubwa iliyonyesha ya mawe ikiwa na upepo mkali iliyo dumu kwa dakika 20.

Mvua hiyo ambayo ilianza kunyesha majira ya saa12:00 jioni siku ya Tarehe 23, Desemba, imesababisha hasara kubwa kwa wakazi wa manispaa ya Singida, jitihada za kumpata mkuu wa wilaya ya Singida Bi Queen Mlozi ili kuelezea tukio hili zimepatikana na kueleza kuwa mpaka sasa nyumba hamsini na moja zimeharibiwa ikiwemo nyumba za watu binafsi na madarasa ya msikiti na kusema kuwa serikali imejipanga kuwasaidia watu walio athirika.

Akieleza diwani wa kata ya mitunduruni Bwana Pantaleo Sorongai amesema mvua iliyonyesha imeleta madhara makubwa na ameomba serikali kutoa msaada wa mahema na chakula kwa wakazi ambao wameathirika kwani hawana sehemu za kujisitiri.

Kwa upande wao wakazi wa manispaa ya Singida wamesema mvua iliyonyesha haijawahi kutokea pamoja na kunyesha muda mfupi imeleta madhara makubwa na wamelalamikia manispaa ya Singida kwa kutokutengeneza vizuri miundombinu ya maji na kusababisha nyumba nyingi kubomoka.