Ijumaa , 24th Jun , 2016

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2016,unaolenga kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali 26 unaopendekeza kufunguliwa kwa Mahakama ya Ufisadi itakayoshughulikia kesia umepitishwa na Bunge.

Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2016, unaolenga kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali 26 unaopendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Ufisadi itakayoshughulikia kesia za Rushwa na Uhujumu Uchumi za kuanzia shilingi bilioni moja.

Akiwasilisha Muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju katika kikao cha 50 cha mkutano wa tatu wa Bunge la 11, Mjini Dodoma amesema muswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa mahakama ya ufisadi itakayokuwa inasikiliza makosa ya uhujumu uchumi na rushwa kubwa zenye thamani ya kuanzisha Shilingi Bilioni Moja tofauti na hivi sasa kesi za uhujumu uchumi zimekuwa zikisikilizwa kama kesi nyingine.

Wakichangia Muswada huo mara baada ya kuwasilishwa leo Bungeni Mjini Dodoma, Wabunge Peter Serukamba wa Kigoma Kaskazini pamoja na Adad Rajab mbunge wa Muheza wamesema bila kuanisha aina ya kesi za kusikilizwa katika mahakama hiyo kutakuwa na mrundikano wa kesi huku wakitaka muundo wake uwe wa kipekee tofauti na mahakama nyingine kwa kuwafikisha watuhumiwa katika mahakama hiyo wenye kesi kubwa ili kuweka utofauti na mahakama nyingine.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ileje, Mhe. Janet Mbene amesema mbali na kuangaliwa kwa aina ya watuhumiwa pia watendaji wa mahakama hiyo ili wasiingie kwenye mkumbo wa kujihusisha na vitendo vya rushwa kama ilivyo katika mahakama nyingine, kufuatia kushindwa kushughulikia kesi za uhujumu uchumi zilizokuwa zinafikishwa katika mahakama hizo.

Akijibu Hoja za Wabunge, ikiwa ni pamoja na hoja ya Jaji Mkuu kufanya uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Ufisadi Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema muundo wa mahakama hiyo itakuwa chini ya Jaji Mkuu na atamshirikisha rais pale itakapobidi.