Jumatatu , 15th Feb , 2016

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni anayegombea tena kuchaguliwa madarakani Alhamisi ijayo amesema anaunga mkono nchi yake kujiondoa kwenye mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia uhalifu ICC iliyoko mjini The Hague Uholanzi.

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni

Museveni aliyeingia madarakani mwaka 1986 alitoa kauli hiyo wakati wa mdahalo wa televisheni uliofanyika jana usiku akishiriki kwa mara ya kwanza katika mdahalo huo na wagombea wengine wa kinyang'anyiro cha urais.

Kiongozi huyo wa Uganda alisema mahakama ya ICC inapendelea na haina usawa na wala haiko makini.

Tangu mahakama hiyo ilipoundwa mwaka 2002 imeanzisha uchunguzi unaozihusisha nchi nane zote kutoka bara la Afrika.

Katika mkutano wa kilele uliopita wa nchi za Afrika mjini Adis Ababa viongozi wa bara hilo waliunga mkono mwito uliotolewa na Kenya wa kutaka nchi hizo zijiondoe katika mahakama hiyo.

Katika uchaguzi mkuu wiki ijayo Museveni atapambana na wagombea wengine saba katika mchuano wa kuwania urais.