Jumanne , 6th Jan , 2015

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo ametoa muda wa siku Tano kwa wakazi wa kijiji cha Ndami na jeshi la jadi Sungusungu wilayani kwimba, kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, aliyepotea.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo ametoa muda wa siku Tano kwa wakazi wa kijiji cha Ndami na jeshi la jadi Sungusungu wilayani kwimba, kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emanuel akiwa hai au amekufa ikiwa ni pamoja na wahusika wa tukio hilo kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Agizo hili la mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo, linakuja kufuatia watu wasiojulikana kumuiba mtoto Pendo Emanuel mwenye ulemavu wa ngozi majira ya saa 4 usiku Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika kijiji cha Ndami na kutoweka naye kusikojulikana.

Mkasa huo umeilazimu kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza kuapa kuwa serikali haitalala usingizi mpaka mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne apatikane.

Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa Mwanza Alfred Kapole amesema kuwa miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa mahakamani zikihusu mauaji ya walemavu wa ngozi, ni kesi tatu pekee ndizo zilizotolewa hukumu mpaka sasa, huku akiilaumu ofisi ya mkemia mkuu wa serikali pamoja na mahakama kwa kuchelewesha kesi hizo.

Mama mzazi wa mtoto Pendo, Bi. Sophia Juma pamoja na mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Chiriko Bi. Specioza Kasoli wamesema kila mtu ana haki ya kuishi na kulindwa.

Ameongeza kuwa mtoto huyo ni kati ya watu 74 wenye ulemavu wa ngozi wilayani Kwimba na alikuwa ni mtu wa 9 kwa kupatiwa ulinzi.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Valentino Mlowola amesema tayari askari polisi wamepiga kambi katika kijiji hicho kwa kazi moja tu ya kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, lakini pia watuhumiwa wanasakwa kwa udi na uvumba ili wafikishwe mahakamani kwa kosa la jinai.