Jumatano , 31st Jan , 2018

Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Muhas, kwa mara ya kwanza kimeandaa mtaala wa shahada ya mwanzo ya wauguzi watakaoshughulikia wagonjwa watakaopata dawa za usingizi kabla na baada ya upasuaji ili kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya, amesema, kabla ya mtaala huo kupitishwa hapo nyuma wagonjwa walikuwa wanapata huduma ya dawa za usingizi pindi wanapohitaji kufanyiwa upasuaji kutoka kwa wataalamu waliopata mafunzo kwa mwaka mmoja au waliojifunza kwenye sehemu zao za kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo wa Shahada za Mwanzo wa Muhas, Prof. Mainem Moshi, amesema, tayari wameshapeleka mtaala wa wahandisi wa vifaa tiba kwani wanahitajika takribani wahandisi vifaa tiba elfu 8 nchini.
Mbali na hayo Dkt  Ulisubisya amekitaka Chuo cha Afya Muhimbili kisisubiri matatizo kutoka kwa wananchi bali wajitahidi kuwa wavumbuzi ili kuisaidia jamii.