Baadhi ya majeruhi wa ajali ya barabarani iliyotokea juzi wakiwa katika wodi ya hopitali ya wilaya ya Mufindi
Serikali imeombwa kutazama uwezekano wa kujenga jengo la wodi ya dharura katika hospitali ya wilaya ya Mufindi na kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba na wataalam wa kutosha ili kuokoa maisha ya watu wanaojeruhiwa katika ajali mbalimbali zinazotokea kwenye barabara ya Tanzam inayotokea jijini Dar es salaam kuelekea nchini Zambia.
Kaimu mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya wilaya Mufindi mkoani Iringa Dkt Idd Omari ametoa ombi hilo kufuatia mzigo mkubwa unaobebwa na hospitali hiyo ambayo ipo kando kando ya barabara ya Tanzam na hivyo kupokea majeruhi wa ajali wa mara kwa mara pamoja na maiti wanaofariki katika ajali za barabarani hali inayoleta changamoto ya namna ya kuhudumia majeruhi pamoja na kuhifadhi maiti kutokana na miundombinu duni.
Kutokana na changamoto ya ongezeko la ajali za barabarani mkoani iringa nimezungumza na mmoja wa wadau mkoani hapa ambaye ni mtaalam wa majanga na maafa mwalimu Creptone Madunda ambaye anaeleza kuwa serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa ina wajibu sasa wa kupanua shughuli zake hadi ngazi ya kata huku pia akisema jeshi la polisi linahitajika kuongeza umakini kusimamia sheria za barabarani ili kudhibiti ajali hizo.
Mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Robert Salim amesema majeruhi 26 kati ya 30 waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi wameruhusiwa na wale wanne waliohamishiwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa wawili kati yao wanaendelea vizuri na wawili bado hali zao siyo nzuri na wanaendelea na matibabu.

