Jumanne , 27th Aug , 2024

Mwanamke mmoja mkazi wa Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, amemuomba Waziri wa maendeleo ya Jamii, Dkt. Doroth Gwajima pamoja na Serikali kwa ujumla kumsaidia kupata haki ya mtoto wake wa kike wa miaka 7, aliyelawitiwa na mwanaume wa miaka 38.

Mama ambaye mwanaye amelawitiwa

Ameiambia EATV mtuhumiwa huyo alikiri kufanya kosa hilo lakini cha ajabu Mahakama imemuachilia huru.

“mara tu ya kugundua mtoto wangu kafanyiwa ukatili nilipomuuliza alimtaja huyo mwanaume na nilipomfata kumuuliza alikiri kutekeleza tukio hilo la kikatili na hata alipofika Polisi alikiri kutekeleza tukio hilo lakini aliomba asamehewe kutokana alitenda kwa kutotarajia, lakini ameshangaa Mahakama imemuachia huru mwanaume huyo”, Mama wa mtoto.

Kisheria mtu anaposhindwa kukubaliana na maamuzi ya Mahakama anatakiwa afanyeje?
“Cha kwanza anatakiwa akate rufaa kwa muda uliowekwa na utafute wanasheria ambao wanaweza kukusaidia kupata haki ambayo unahisi hukuipata kupitia Mahakama na baada ya hapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa upya na kupitiwa baadhi ya vielelezo ambavyo vitasaidia kupata ushahidi wa kesi husika”, akisema Anna Henga, Mkurugenzi LHRC.

Nao baadhi ya wadau wa haki za binadamu wameishauri Serikali kufanya mapitia ya sera kuhusu upatikanaji wa haki za binadamu.
“Ili kupunguza malalamiko Serikali inahitaji sana kuongeza taasisi kama Takukuru kwa ajili ya usimamizia wa kesi ili kupunguza mianya ya Rushwa ambayo imekuwa ikisababisha watu wengi kukosa haki zao kutokana na hali zao za kiuchumi”, alisema  Delina Kafuko-Mdau wa haki za binadamu.

“Nafikiri kwenye ripoti ya haki jinai kuna mapendekezo yamewekwa kwa ajili ya kupata haki kwa wahanga nafikiri Serikaliningeifanyia kazi ingeleta majibu chanya lakini pia kungekuwepo na chombo huru ambacho kinaisimamia utoaji wa haki hasa Polisi na Mahakamani ili kuondoa hizi changamoto”, alisema Fundikila Wazambi, Mdau wa Haki za Binadamu.

Awali wakati tukio linaripotiwa kupitia mitandao ya kijamii ya EATV na EARADIO , Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Dokta Doroth Gwajima alioneshwa kuguswa na tukio hilo na kumpa Mwanasheria kwa ajili ya usaidizi wa kisheria ambapo leo Agost 27, 2024 wamekata rufaa ya kesi hiyo.