Alhamisi , 25th Mei , 2017

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku Musukuma amesema hawezi kumsifia hata kidogo Prof. Jumanne Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii kwani yeye na watu wake wa Wizara wanafanya mambo ya ajabu hasa kwa watu wa Kanda ya Ziwa.

Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita

Musukuma anasema watu wa Wizara ya Maliasili wamekuwa wakiuza ng'ombe za watu jamii ya wasukuma na kuzipiga mnada kwa dili kwa lengo la kujinufaisha wenyewe, hivyo mbunge huyo amesema wasukuma wameamua kuwa wataziroga ng'ombe zote ili wanaokula ngo'mbe hizo Dar es Salaam wavimbe matumbo. 

"Napata shida sana kujiuliza labda sisi watu wa kanda ya ziwa labda tulikuja kwa bahati mbaya Tanzania hii, mbona yanayofanyika Kanda ya Ziwa hayafanyiki Kanda ya Kaskazini wakati nao wana mapori, Waziri ametoa siku tatu tukamatiwe ng'ombe kwa kisingizio kwamba ni ng'ombe za Wanyarwanda wakati huo huo watumishi wake wanaowaingiza Wanyarwanda wanawaambia toeni ng'ombe, mnaenda kukamata ng'ombe za Wasukuma halafu unazipiga mnada na mnada wenyewe unavyopigwa ni wa dili" alisisitiza Musukuma 

Mbunge huyo aliendelea kuelezea namna watu wa Wizara ya Maliasili wanavyofanya minada hiyo huku wakiwaumiza wafugaji

"Yaani ng'ombe 600 unaambiwa ulete milioni tatu halafu wanatoa watu wao wa Ubungo sasa hapo nikupongeze kwa sababu gani? Tunajua mipango inayoendelea kwenye wizara yako na niliwapigia kabisa watumishi wako, wananiambia mliipenda wenyewe kwa kauli yake kama Mwenyekiti wa Chama kesho yake akapiga ng'ombe za watu mnada yaani ng'ombe 500 zinauzwa milioni tatu" alisema Musukuma 

Joseph Msukuma aliendelea na msimamo wake 

"Nataka nikwambie sisi Wasukuma sasa tumeamua na ninazungumza uelewe tutaziroga hizo ng'ombe mtavimba matumbo mnaozila huko Dar es Salaam, haiwezekani kwanini wanunuzi watoke Dar es Salaam peke yake yaani leo siku ya mnada watu wametoka na malori Pugu wamejuaje kama wanakuja kushinda kwenye minada. Mnatukamatia ng'ombe hivi hii serikali imekosa sehemu ya kukusanya hela mpaka mkanyang'anye ng'ombe za wafugaji haiwezekani Mh. Maghembe"