Ijumaa , 29th Jan , 2016

Watu zaidi ya 1,000 wamevamia msitu wa hifadhi ya Taifa ya Rwamgasa katika wilaya za Geita na Mbogwe mkoani Geita na kuendesha uchimbaji madini aina ya dhahabu na kusababisha uharibifu.

Baadhi ya Wananchi waliovamia Mgodi wa Geita

Aidha imeelezwa kuwa dhahabu inayozalishwa na wavamizi hao wa uchimbaji madini huishia mikononi mwa walanguzi na hivyo serikali kupoteza mapato na rasilimali hiyo.

Meneja Wakala wa huduma za misitu Wilaya ya Geita Shadrack Msilu amesema Ofisi yake imetoa Siku saba toka jana kwa Wavamizi hao kuwa wamejiondoa wenyewe baada ya muda huo nguvu za dola zitatumika na tayari taarifa zimepelekwa kwa mamlaka husika.

Erasto Majula ni Afisa mtendaji wa kijiji cha Rwamgasa anatetea Uvamizi huo kwa kuiomba Serkali kuweka utaratibu mzuri wa kusimamia uchimbaji huo kwa mujibu wa sheria badala ya kuwafukuza kutokana na kukosa maeneo ya uchimbaji mdogo.

Hata hivyo utetezi wake umepingwa na wadau wa sekta ya Mazingira kwa madai kutaathiri mazingira licha ya utoroshwaji dhahabu kutokana na kutokuwepo kwa Uongozi kwa mujibu wa sheria katika Hifadhi hiyo.

Wakati huohuo Mgogoro kati ya Rwamgasa Saccoss Golmine na mchimbaji Nassor Juma wa kugombea umilki wa kiwanja alichomilkishwa kisheria awali Nassor Juma umemalizika baada ya kuridhia kufanya kazi kwa pamoja na leseni ya Umilki kuandikwa kwa jina laSaccos.