Jumatatu , 27th Aug , 2018

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu impatie muda wa wiki tatu ili atafute wakili mwingine kwa kuwa Wakili wake Jeremiah Mtobesya amejitoa.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.

Msigwa pamoja na vongozi wenzake wanane wa (Chadema) akiwamo Mwenyekiti wao Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo uchochezi na kufanya mkusanyiko usiohalali.

Kwa pamoja viongozi hao walipaswa kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, lakini imeshindikana kwa sababu mshtakiwa wa tano, Esther Matiko ambaye mbunge wa Tarime Mjini anaumwa.

Naye Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa Msigwa kwa sasa hana wakili kwani awali alikuwa akitetewa na wakili Jeremiah Mtobesya ambaye amejitoa, baada ya kueleza hayo Kibatala, Msigwa alinyoosha mkono na kuieleza Mahakama kuwa impatie muda wa wiki 3 ili aweze kutafuta wakili mwingine.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, mwaka huu ili washtakiwa wasomewe maelezo yao ya awali, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendajia jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es salaam.