Jumatano , 20th Mei , 2015

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu na Balozi wa falme za kiarabu hapa nchini, Abdallah Al Suweid jana wamekabidhi kwa wananchi mradi wa visima 33 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.83 vilivyochimbwa katika wilaya ya Ngorongoro

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu

Aidha visima hivyo vitanufaisha wananchi zaidi ya 200,000 wa Wilaya hiyo, ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji kwa zaidi ya miaka 30.

Akizungumza katika kata za Oloirien Magaiduru na Ololosokwani katika tarafa ya Loliondo wilayani humo. waziri Nyalandu ameomba wananchi hao kulinda visima hivyo kwa manufaa ya umma.

Amesema kukamilika kwa mradi huo ni matokeo ya mahusiano mema kati ya serikali na wawekezaji katika wilaya hiyo na kumaliza matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya wananchi wa jamii ya wafugaji.

Nyalandu amesema ni vema wananchi wakaheshimu wawekezaji na wawekezaji wakaheshimu wananchi ili kudumisha mahusiano mazuri na kumaliza migogoro.

Kuhusu suala la migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo amesema inachangiwa na kukaribishwa wafugaji kutoka nchi jirani jambo ambalo lazima likomeshwe mara moja.

Naye balozi Al Suweid amesema kukamilika kwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kusaidia jamii katika awamu ya kwanza na miradi mingine itaanzishwa kwa manufaa ya jamii ya Loliondo.

Balozi Alsuweid amewataka miradi hiyo ya visima virefu vilivyofungwa mitambo ya umeme wa jua kuvuta maji, kutunzwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo na pia maeneo yaliyotengwa kwa ajili mifugo kupata maji.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa miradi hiyo, diwani wa kata ya Ololosokwani Iyanick Ndoinyo na diwani wa kata ya Oloilein Magaidulu Mohamed mmarekani, wamepongeza kampuni ya OBC kwa msaada huo mkubwa.

Ndoinyo amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutapunguza tatizo la akina mama na watoto pamoja na mifugo kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.

Diwani mmarekani amesema wananchi waliokabidhiwa miradi hiyo, watahakikisha wanailinda na kuitunza ili iendelee kuinufaisha jamii ya Loliondo yenye matatizo makubwa ya maji.