
Mamlaka za mji huo zimesema Alhamisi kuwa takriban watu 11 hawajulikani waliko.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imesema vifo vya zaidi ya watu 60 vimetokana na kukosa hewa katika moto huo uliotokea Jumatano jioni. Miili ya watu 14 iliyoteketea vibaya bado haijatambuliwa.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, timu za ulinzi wa raia zimefanikiwa kuwaokoa zaidi ya watu 45 waliokuwa wamekwama ndani ya jengo. Licha ya kuwa moto umedhibitiwa, bado juhudi za kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana waliokuwemo kwenye jengo hilo zinaendelea. Eneo hilo la maduka lililozinduliwa mapema wiki hii lenye ghorofa tano lilikuwa pia na migahawa.
Kutokana moto huo Gavana wa al Kut, Mohammed al-Mayyeh ametangaza siku tatu za maombolezo. Amesema chanzo cha moto bado kinaendelea kuchunguzwa lakini mmiliki wa jengo amefunguliwa kesi. Hata hivyo hakukutolewa ufafanuzi wa madai ya kesi hiyo
Matokeo ya uchunguzi wa awali yanatarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 kwa mujibu wa shirika la habari la nchini humo INA. Licha ya maelezo hayo, mmoja wa waliosalimika ameliambia shirika la habari la AFP moto ulisababishwa na kulipuka kwa kiyoyozi kimoja.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani katika taarifa yake, amemuagiza waziri wa mambo ya ndani kwenda kwenye eneo la tukio kufanya uchunguzi na kuchukua hatua ili kuzuia tukio kama hilo lisitokee tena.