Kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo akiwa ametembelea soko la Masasi lilitoeketea kwa moto.
Akizungumza na East Africa Radio kutoka wilayani humo kwa niaba ya kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, kamishina msaidizi wa polisi Japhet Kibona, amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika kwa haraka lakini wanaendelea na utafiti ili kuweza kubaini.
Aidha, amesema moto huo ulioanza majira ya saa nne usiku, umeteketeza soko lote na kiasi kikubwa cha mali ambazo bado hazijafahamika thamani yake zimeteketea, na kwamba zilizookolewa ni chache kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kurahisisha kuuzima.
Amesema wilaya hiyo haina gari kubwa la zima moto na yaliyopo ni madogo ambayo hayana matenki ya akiba ya kuhifadhia maji, hivyo kushindwa kufanikisha zoezi la uzimaji ambapo wananchi walijaribu kuzima kwa kutumia michanga na ndoo za maji.
Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Mh. Zitto Zuberi Kabwe ambaye alikuwa ziarani mkoani humo alitembela soko hilo kushuhudia madhara na hasara walioipata wafanyabiashara wa soko hilo.