Jumamosi , 28th Feb , 2015

Wekundu wa Msimbazi Simba SC imefanikiwa kurejesha heshima na kutuliza nyoyo za mashabiki wake baada ya kuitungua Tanzania Prisons jumla ya mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo uliochezesha na mwamuzi Jacob Adongo wa Mara, hadi mapumziko tayari Simba SC ilikuwa mbele kwa mabao 3-0 yote yakifungwa na Mshambuliaji Ibrahi Salum Ajibu.

Hajibu alifunga bao la kwanza dakika ya 15 akimalizia pasi nzuri ya Mganda, Dan Sserunkuma ambaye alimlamba chenga beki wa Prisons Nurdin Chona kabla ya kumpasia mfungaji aliyemchambua kipa Mohamed Yussuph.

Bao la pili Hajibu alifunga dakika ya 21 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mohamed Yussuph kufuatia shuti la mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.

Hajibu alikaribia kukamilisha Hat-Trick mapema dakika ya 24 baada ya kupiga mpira wa adhabu uliookolewa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Lakini mchezaji huyo zao la Simba B akatimiza ndoto zake za Hat-Trick dakika ya 41 baada ya kufunga kwa penati, kufuatia beki wa Prisons Lugano Mwangama kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Kipindi cha pili, Simba SC waliendelea kuutawala mchezo na kupata mabao mawili zaidi yaliyofungwa na Mganda Emmanuel Okwi na Ramadhan Singano Messi. Okwi alianza kufunga dakika ya 75 akifumua shuti kali baada ya kupokea pasi ya beki wa kushoto Mohammed Hussein Tshabalala na Messi akakamilisha dakika ya 84 akimalizia Krosi ya Okwi.

Awali katika Dakika ya 68, Nurdin Chona wa Prison alitolewa nje kwa kadi ya pili ya njano baada ya kumtolea maneno machafu mwamuzi Adongo.

Ushindi huu umetuliza nyoyo za mashabiki na wanachama wa Simba ambayo kesho (Jumapili Machi 1) itafanya mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo.

Wakati huo huo Simba imepata pigo lingine kwa kuondokewa na mchezaji wao wa zamani Zuberi Magoha aliyefariki na kuzikwa leo jijini Dar es salaam.

Mjini Shinyanga pambano kati ya Stand United na Kagera Sugar limevunjika kutokana na mvua kubwa kunyesha na kusababisha uwanja wa Kambarage kujaa maji hali iliyosababisha mwamuzi kuahirisha mchezo katika dakika ya 80.

Wakati mchezo huo unaahirishwa, Stand United ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Mnigeria Abaslim Chidiabele kwa njia ya penati baada ya yeye mwenyewe kuchezewa madhambi katika dakika ya 45.

Mchezo huo utarudiwa kesho asubuhi kwa dakika 10 zilizobaki.

Matokeo mengine ni kwamba Coastal Union imeifunga Mgambo JKT 1-0 lililofungwa na Mganda Yayo Lutimba katika dakika ya 88.
Mkoani Mbeya Timu ya Mbeya City imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting.

Kwa matokeo haya Simba imefikisha point 23 nafasi ya 4 sawa na Ruvu Shooting huku Coastal Union ikifikisha point 22 nafasi ya 6, Mbeya City point 18 nafasi ya 12, Mgambo imebaki katika nafasi ya 13 ikiwa na point 17 na Prisons nafasi ya 14 (mkiani) ikiwa na point 12.