Jumamosi , 3rd Jan , 2015

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iramba Bi. Halima Mpita amekumbwa na hali ya taharuki baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu lililowekwa katika mfumo wa zawadi aliyoipokea kutoka kwa wadau.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Singida ACP Thobias Sedoyeka

Jeshi la polisi mkoani Singida limeamua kuagiza wataalamu wa mabomu kutoka jeshi la wananchi mkoani Arusha kwa ajili ya kuchunguza na kubaini kitu ambacho kinasadikiwa kuwa bomu ambalo lilimlipukia mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iramba Bi. Halima Mpita.

Akieleza kwa waandishi wa habari huku akionesha mabaki ya bomu hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Singida ACP Thobias Sedoyeka amesema tukio hilo ambalo limetokea siku ya tarehe 2 Januari, 2015 baada ya mkurugenzi huyo, kupewa zawadi ya mwaka mpya kutoka kwa katibu muhtasi wake, aliyoipokea kutoka kwa wadau wake. 

Akieleza zaidi kamanda Sedoyeka amesema baada ya kupeleka zawadi hiyo nyumbani kwake aliyopewa siku ya tarehe 30 Disemba, 2014 na kuamua kuifungua tarehe 2 Januari, 2015 na kulipuka, ulikuwa na ujumbe unaosema “Hatuwezi kufanya dili ya shilingi milioni 90 halafu ukatudhurumu”.
 
Jeshi la polisi mpaka sasa bado hawajafanikiwa kumshika mtu aliye husika na tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea, ili kuweza kuwabaini walio husika na kuchukuliwa hatua kali za sheria.