Ijumaa , 10th Jun , 2022

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za ruzuku ya mafuta ambayo ni shilingi bilioni 100 na kusababisha bei ya mafuta kushuka, na kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema

Mjema ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

"Wananchi wa Shinyanga niwaambieni Rais wetu anatupenda sana, ameona wananchi wake wanateseka kwa kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali yakiwamo mafuta, ikabidi akae na watalaam wake na kisha kutafuta pesa na ameweka Sh.bilioni 100 kwenye Ruzuku ya mafuta na sasa yameshuka bei, nani kama Rais Samia," amesema Mjema.

Aidha, amesema katika mkoa huo wa Shinyanga Rais Samia ametoa fedha nyingi, na kutekelezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya elimu, afya, umeme, maji, kilimo, miundombinu ya barabara, pamoja na kutoa fedha Sh. bilioni 15 kujenga uwanja wa Ndege Ibadakuli, na sasa bilioni 3.5 zimeshaanza kufanya kazi na mkandarasi yuko kazini.