Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameridhia kutoa jumla ya Shilingi Milioni 400, zinazotumika kukamilisha ujenzi wa shule ya Sekondari Eyasi Wilayani Karatu Mkoani Arusha, shule inayotajwa kuwa Mkombozi wa Elimu kwenye Tarafa hiyo ya Eyasi.
Wakati wa ukaguzi wa Ujenzi huo, Mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu Ndugu Juma Hokororo, Wananchi wa Kata hiyo wamemshukuru Rais Samia kwa Ujenzi huo, wakisema watoto walikuwa wakisafiri umbali mrefu wa zaidi ya Kilometa 24 kufuata shule ilipo, lakini sasa ujenzi wa shule hiyo na Mabweni utaondoa adha kubwa waliyokuwa wakiipata wanafunzi hao.
Kwa Upande wake Ndugu Hokororo amemshukuru Rais Samia pia kwa kuendelea kuikumbuka Karatu katika miradi tajika ya huduma mbalimbali za kijamiii, akiahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili fedha inayotumika iende sambamba na thamani yake sambamba na kufikiwa kwa ubora uliokusudiwa kwenye miradi hiyo.
Ujenzi wa Shule ya Sekondari Eyasi unatekelezwa na serikali kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP) na kugharimu zaidi ya Milioni 584 za awali kwa ujenzi wa madarasa, Ofisi za waalimu, maabara na matundu ya vyoo.