Alhamisi , 28th Jan , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametolea ufafanuzi wa katazo la vyama vya siasa vilivyoshindwa kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi na kusema hakuna chama kilichokatazwa kufanya mikutano ya kisiasa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majiliwa

Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Mhe. Freeman Mbowe Waziri Mkuu amesema kuwa serikali inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na katiba hivyo inatambua kuwa katika mfumo wa vyama vingi vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano ila kwa utaratibu maalum.

Waziri Majaliwa amesema kuwa mwandishi aliyemnukuu kuhusiana na kauli hiyo hakumtendea haki kwa kuwa aliitoa akiwa kama mbunge wa kawaida na si waziri mkuu na yalikuwa ni makubaliano ya vyama vya siasa katika jimbo lake.

Waziri mkuu huyo ameongeza kuwa kauli hiyo aliitoa wakati alipokutana na madiwani na viongozi wengine wa mkoa wake ambapo walikubaliana kuweka siasa pembeni na kufanya kazi kwa pamoja katika kuleta maendeleo.