Alhamisi , 6th Feb , 2025

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo February 6, 2025 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ghala la Kisasa la kuhifadhia bidhaa za afya linalojengwa na na Bohari ya Dawa (MSD) katika eneo la Kizota, Mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mhagama amebainisha kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya Afya, na imeendelea kujikita kwenye nguzo zinazo tuongoza za kimfuno zinazopelekea Ubora wa huduma kwenye sekta ya Afya.

"Kazi zilizofanywa zinaonekana, na hata leo tumeona uwekezaji mkubwa wa ghala la hili kubwa na la Kisasa ambalo lina Ubora wa kimataifa, serikali imewekeza hapa zaidi ya Bilioni 23.7" kujenga ghala hili lenye mita za Mraba 7,200. Alisema Mhagama

Mhe. Mhagama ameongeza kuwa ujenzi huo pia umeendelea kwenye Kanda ya Mtwara, ambapo zaidi ya Bilioni 18 zimetumika kukamilisha ujenzi, huku akibainisha kwamba ujenzi huo pia utaendelea katika Kanda nyingine za MSD ambazo ni Mwanza, Chato, Iringa, Moshi, Arusha na Songea.

"Lengo kubwa la jitihada hizi ni kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati na kwa Ubora unaotakiwa, na zinahifadhiwa katika mazingira yanayotakiwa, hivyo Bodi, menejimenti na Serikali ya Dkt. Samia mmeupiga mwingi. Alisisitiza Mhe. Mhagama.

Katika hatua nyingine Mhe. Mhagama ameupongeza uongozi wa MSD kwa kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo amebainisha kwamba hivi sasa upatikanaji huo umepanda hadi kufikia asilimia 83%.

Ameongeza kuwa MSD ni nyenzo muhimu katika uimarishaji wa huduma za afya katika taifa letu.

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na MSD Ili kuhakikisha ndoto na maono haya ya kumkomboa mtanzania, na kuweka usalama kwenye taifa letu yanatimia, kwani afya ya Mtanzania ni usalama wa taifa letu.