Jumatano , 5th Mar , 2025

Vikosi vya Sudan Kusini vimemkamata waziri wa mafuta na maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi wanaoshirikiana na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar wakati wanajeshi wakizingira nyumba yake katika mji mkuu Juba.

Naibu mkuu wa jeshi, Jenerali Gabriel Duop Lam, mfuasi wa Machar, alishikiliwa Jumanne, wakati Waziri wa Petroli Puot Kang Chol alikamatwa Jumatano pamoja na walinzi wake na familia yake.

Hakuna sababu iliyotolewa ya kukamatwa kwa watu hao, ambayo imekuja baada ya kundi lenye silaha linaloshirikiana na Machar kuvamia kambi ya jeshi katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Upper Nile.

Machar, ambaye ushindani wake wa kisiasa na Rais Salva Kiir katika siku za nyuma ulilipuka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, alisema mwezi uliopita kwamba kufukuzwa kwa washirika wake kadhaa kutoka kwenye nyadhifa katika serikali kunatishia makubaliano ya amani ya 2018 kati yake na Kiir.

Makubaliano hayo yamemaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano ambapo zaidi ya watu 400,000 waliuawa. Waziri wa maji Pal Mai Deng, msemaji wa chama cha Machar cha SPLM-IO, alisema kukamatwa kwa Lam kunaweka makubaliano yote ya amani hatarini.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Desemba 2013 baada ya Kiir kumfuta kazi Machar pia vilisababisha zaidi ya watu milioni 2.5 kuyahama makazi yao na kuwaacha karibu nusu ya taifa hilo lenye watu milioni 11 wakihangaika kutafuta chakula cha kutosha.

Mvutano huo unaonekana kuchochewa na kuongezeka kwa wasiwasi juu ya machafuko katika eneo la Upper Nile.