Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za kijamii toka Ofisi ya Taifa Takwimu NBS Ephrahim Kwesigabo
Mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Mei Mwaka huu umepanda kwa asilimia 0.8 hadi kufikia asilimia 5.3 kutoka asilimia 4.5 kwa mwezi April huku kushuka kwa thamani ya shilingi kukitajwa kuwa moja ya sababu kubwa.
Akitoa Takwimu hizo leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za kijamii toka Ofisi ya Taifa Takwimu NBS Ephrahim Kwesigabo amesema kuwa kupanda huko kwa mfumuko wa bei pia kumetokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma.
Amesema mfumuko huo katika bidhaa kama za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 8.5 toka asilimia 7.1 mwezi Aprili, kwenye migahawa pia bei zimepanda kwa 4.1% bei za nguo za wanaume kwa asilimia 5.6 nyumba za kulala wageni kwa 4.2%.
Aidha katika unga wa Muhogo mfumuko umepanda kwa asilimia 12.3, samaki kwa asilimia 11.7 na choroko kwa asilimia 13.9 pamoja na bei za Petrol kwa asilimia 5.8 na dizeli kwa asilimia 3.2.
Kwesigabo ameongeza kuwa Uwezo wa shilingi mia moja kununua bidhaa na huduma kwasasa imeshuka hadi kufikia shillingi 63.35 toka 63.61 ilivyokuwa April 2015.