Jumatano , 16th Dec , 2015

Jeshi la polisi mkoani Singida linamshikilia mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Itaja na mkewe kwa tuhuma za kumfungia ndani ya chumba mtoto wao mlemavu wa viungo kwa miaka 12 bila kutoka nje.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema tukio hilo liligundulika juzi katika kijiji hicho baada ya Polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa wasamaria, na kuwataja watuhumiwa kuwa ni David Mtipa (59) ambaye ni Mchungaji wa Kanisa hilo na mkewe Mariam Philipo (45) wote wakazi wa kijiji cha Itaja katika tarafa ya Mgori wilayani Singida.

Akielezea tukio hilo Kamanda Sedoyeka alisema watuhumiwa walimfungia ndani ya chumba mtoto Timotheo David (30) kwa muda wa miaka 12 huku huduma zote za kibinadamu, ikiwemo haja ndogo na kubwa pamoja na chakula zikifanyika humo humo ndani.

“Baada ya timu ya askari wa upelelezi na ofisa ustawi wa jamii kufika eneo hilo wakiwa na viongozi wa kijiji na kufanya mahojiano, watuhumiwa walikiri kumfungia chumbani mtoto wao huyo na kwamba ni mlemavu wa miguu na mikono, lakini pia ni mlemavu wa akili,” alisema Kamanda Sedoyeka.

Kwa mujibu wa Kamanda Sedoyeka mtoto huyo alizaliwa mwaka 1984 akiwa mzima, lakini alipofika darasa la sita 2003 alianza kuugua ugonjwa usiojulikana ikiwa ni pamoja na kuanguka kisha kutoa povu mdomoni, huku mwili wake ukibadilika rangi kuwa ya njano na kutibiwa bila mafanikio.

Aidha, alisema mlemavu huyo alitibiwa maeneo mbalimbali bila mafanikio na ndipo wazazi hao walipoamua kumfungia ndani baada ya kuona wanafedheheshwa mbele ya jamii huku akila chakula, kujisaidia humo chumbani na kutoruhusiwa kutoka nje.

Kwa sasa mtoto huyo amepelekwa hospitali ya mkoa wa Singida kwa matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake wakati wazazi hao wakishikiliwa na kuhojiwa ili hatimaye wafikishwa mahakamani kwa vitendo vya ukatili.