Alhamisi , 19th Dec , 2019

Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, amechaguliwa kwa mara nyingine tena kuongoza kiti cha Uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kupata ushindi wa kishindo kwa kupigiwa kura 886 na kumburuza mgombea mwenzake, Cecil Mwambe aliyepata kura 56 pekee.

Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.

Matokeo ya Uchaguzi huo yametangazwa leo Disemba 19, 2019 na Msimamizi wa Uchaguzi huo Sylvester Masinde, kufuatia uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia leo.

"Bwana Cecil Mwambe amepata Kura 59 sawa na asilimia 6.2, Freeman Aikael Mbowe amepata kura 886, sawa na asilimia  93.5, Kura zilizoharibika ni tatu kwa matokeo haya napenda kumtangaza Freeman Mbowe, kama Mwenyekiti wetu wa chama wa awamu inayokuja" alitangaza Msimamizi wa Uchaguzi, Sylvester Masinde.

Aidha katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, imechukuliwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, ikichukuliwa na Said Issa Mohammed.