Jumanne , 24th Feb , 2015

Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, amesema serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kudhibiti na kupambana na vitendo vya mauaji ya albino hali inayosababisha vitendo hivyo kuzidi kushamiri.

Waziri mkuu mstaafu fredrick sumaye

Akizungumza jijini Mwanza jana wakati wa uzinduzi wa albamu ya watoto wa kanisa la EAGT Lumala mpya, Sumaye amesema vitendo vya baadhi ya watu kuwanyakua watoto wenye ulemavu wa ngozi na kuwaua, ni jambo la kusikitisha na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amesema kwa serikali kutochukua hatua muafaka, kunalisababishia taifa aibu hasa pale inapoonekana baadhi ya wahusika hutumia viungo vya albino kwa ajili ya kutafuta madaraka ama kupata utajiri.

Sumaye amesema kutokana na hali hiyo, serikali na vyombo vya usalama vinatakiwa kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na vitendo hivyo vya kihalifu vinavyozidi kushamiri nchini.

Amesema haiwezi kuingia akilini kwa viungo vya binadamu hasa albino kusaidia kupata umaarufu wa uongozi ama utajiri kama ni wanaotaka hivyo kwanini wasiweze kuuza sehemu ya vingo vyao.

Waziri mkuu mstaafu amesema pesa zinazotolewa na baadhi ya watu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu zinatokana na ubadhilifu wa mali za umma.

Aidha, Sumaye ametoa tahadhari kwa viongozi wanaosimamia michakato ya uchaguzi kutakiwa kutenda haki kwa wagombea na wapiga kura ili kuepukana na machafuko kama yanavyotokea kwa baadhi ya nchi barani barani Afrika.

Awali mchungaji wa kanisa hilo, Daniel Kulola, amesema wamekuwa wakiwalea watoto katika matunzo ya kumtukuza Mungu ili kuepukana na matendo maovu.