Jumanne , 4th Oct , 2016

Utawala bora barani Afrika umeimarika kidogo sana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, wakati kudorora kwa usalama na kutofuata sheria kukirudisha nyuma hatua zilizopigwa katika nyanja nyinginezo kama za haki za kibinadamu na uchumi.

Mo Ibrahim

Ripoti ya utafiti iliyozinduliwa leo na wakfu wa Mo Ibrahim kuhusu utawala bora Afrika imeonesha kwamba nchi za Mauritius, Botswana, na Cape Verde, zimechukua nafasi tatu bora katika utawala bora zikifuatiwa na Ushelisheli na Namibia huku Afrika kusini ikiorodheshwa nambari sita.

Kwa ujumla utafiti huo wa faharasa umeonesha kwamba bara hilo la Afrika limejiongezea pointi moja tu ikilinganishwa na utafiti uliofanywa mwaka 2006 hiyo ikiwa ni miaka kumi iliyopita.

Utafiti huo unaonyesha kuwa katika kila nchi kumi, tatu zimeshuka daraja, huku mataifa yenye uwezo mkuu kiuchumi kama vile Afrika Kusini na Ghana yakipungukiwa zaidi.