Jumatatu , 5th Jan , 2015

Mwanasheria mkuu wa serikali George Masaju amewataka watanzania kujenga imani na serikali yao juu ya masuala mbalimbali ikiwemo ya mikataba hasa inayogusa maslahi ya taifa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju akila kiapo mbele ya Rais Kikwete

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam hafla iliyohudhuriwa pia na makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, waziri mkuu Mizengo Pinda, jaji mkuu wa Tanzania, mkuu wa majeshi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na baadhi ya mawaziri, Mh Masaju ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na ueledi.

Waandishi wa habari wakapata fursa ya kuuliza maswali ambapo miongoni mwake lilihusu suala la usiri wa mikataba mbalimbali inayolalamikiwa na wananchi pamoja na tatizo la rushwa Mh Masaju mbali na kudai kuwa bado hajaingia ofisini lakini ameahidi kushughulikia suala hilo pindi tu atakapoingia ofisini na kupata taarifa.

Kwa mujibu wa Masaju, maeneo ambayo atayaangalia ni pamoja na suala na kilio cha muda mrefu cha wanachi na wabunge la kutaka uwazi katika mikataba mbalimbali ambayo serikali imekuwa akiisaini kwa niaba ya wananchi.

Mh Masaju ameshika wadhifa huo kufuatia kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu wa serikali aliyekuwepo Jaji Frederick Werema mwezi Desemba mwaka jana kutokana na kashfa ya ufisadi ya Escrow ambapo awali kabla ya uteuzi wake alikuwa Naibu Mwanasheria mkuu wa serikali.