
Kupitia televisheni ya taifa Msemaji wa utawala wa kijeshi wa Gabon amesema kwamba wameamua mara moja kufungua tena mipaka ya nchi kavu, baharini na anga kuanzia Jumamosi.
Kundi la wanajeshi 12 wa Gabon walitangaza siku ya Jumatano kwamba mipaka ya nchi hiyo imefungwa hadi itakapotangazwa tena katika taarifa iliyotangazwa kwenye kituo cha televisheni cha Gabon 24.
“Mipaka ya nchi kavu, baharini na angani ilifunguliwa kwa sababu serikali ya kijeshi ilijali kuhifadhi heshima ya utawala wa sheria, uhusiano mzuri na majirani zetu na mataifa yote ya ulimwengu na ilitaka kutimiza ahadi zake za kimataifa", Msemaji wa jeshi alisema
Maafisa wa kijeshi wakiongozwa na Jenerali Brice Oligui Nguema walichukua mamlaka siku ya Jumatano na kumweka Bongo katika kizuizi cha nyumbani na kumteua Nguema kama mkuu wa nchi na hivyo kumaliza miaka 56 ya familia ya Bongo madarakani.
Mapinduzi hayo ya nane katika Afrika Magharibi na Kati katika kipindi cha miaka mitatu yameibua wasiwasi kuhusu kuenea kwa uchukuaji mamlaka wa kijeshi katika kanda nzima hivyo kufuta maendeleo ya kidemokrasia yaliyopatikana katika miongo miwili iliyopita.
Viongozi wa mapinduzi wamekuwa chini ya shinikizo la kimataifa kurejesha serikali ya kiraia lakini wamesema kwamba hawatakimbilia kufanya uchaguzi.