Jumatano , 9th Nov , 2016

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kupitia kikosi chake maalum cha kupambana na ujambazi wa silaha limefanikiwa kuwatia mbaroni watu watatu kwa kosa la kula njama ya kuiba zaidi ya shilingi milioni 200 huku wakiwa na bastola bandia.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam CP Simon Sirro

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam CP Simon Sirro amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya askari kupokea taarifa kutoka kwa msiri juu ya watu hao kutaka kufanya uhalifu huo kwa kuteka gari ambalo limebeba kiasi cha fedha  hizo.

Mbali na hilo jeshi hilo pia limekamata watuhumiwa wawili kwa makosa ya wizi wa magari manne yaliyoibiwa Jijini Dar es Salaam na kukamatwa katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Tabora ambapo magari hayo yalipelekwa mikoa hiyo kwa ajili ya kuuzwa.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata zaidi ya watuhumiwa mia nne kwa makosa mbalimbali ya kihalifu Jijini Dar es Salaam yakiwemo makosa ya wizi wa vifaa vya magari, kucheza kamari, unyang’anyi wa kutumia nguvu pamoja na kutengeneza pombe bandia.

Hata hivyo jeshi hilo kupitia kikosi chake cha usalama barabarani limekusanya zaidi ya shilingi milioni 40 kupitia tozo za makosa ya usalama barabarani.