Ijumaa , 16th Jul , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametaja mambo manne yaliyopelekea yeye kufanya ziara ya siku mbili nchini Burundi, likiwemo suala la kutoa shukrani kwa namna nchi hiyo ilivyokuwa mfariji kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Magufuli.

Rais Samia Suluhu Hassan, akikagua gwaride la Jeshi la Jamhuri ya Burundi alipowasili Ikulu Ntare House Jijini Bujumbura Burundi

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 16, 2021, Ikulu ya Burundi, wakati alipokaribishwa kuwahutubia wana Burundi pamoja na Watanzania kwa ujumla na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, ambapo pia ametaja mambo mengine ikiwa ni pamoja na kutoa pongezi kwa Taifa hilo huku jambo lingine likiwa ni kujitambulisha kwani yeye ni Rais mgeni kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

"Sababu ya Nne nimekuja Burundi kwa lengo la kukuza na kuendeleza uhusiano mzuri wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema uliopo kati ya mataifa yetu mawili, kama mnavyofahamu nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri wa enzi na enzi sio tu wa kisiasa lakini wa kidamu," amesema Rais Samia