Makamu wa Rais Samia Suluhu akimpa pole mjane wa Marehemu Benjamin Mkapa Mama Anna Mkapa.
Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amewaongoza viongozi mbalimbali wa kiserikali wakiwemo mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, viongozi wa taasisi za serikali pamoja na mamia ya wananchi katika siku ya pili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu hayati Benjamin Mkapa aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24.
Hapa ni uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam Viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi pamoja na wananchi wakiwa wamefika katika zoezi la kutoa heshima za mwisho na kuaga mwili hayati Mkapa ambapo baadhi ya wakuu wa mikoa wamezungumzia jinsi walivyomfahamu kiongozi aliyekuwa lulu na hazina kubwa ya taifa.
Katika moja ya kitengo kilichoanzishwa na serikali ya Mkapa ni Habari, Mawasiliano na Uhusiano, ambapo wakiongea na EATV SAA 1 maafisa habari serikalini wamesema uwepo wao serikalini unaonesha uwazi wa utoaji wa taarifa za Serikali ambalo ndiyo ulikuwa msingi wa kuanzishwa kwake
Serikali ilitangaza siku saba za maombolezo huku siku ya kesho Rais wa Tanzania Dk John Magufuli akitarajiwa kuwaongoza viongozi wakuu wa kitaifa pamoja na viongozi wa kimataifa kuaga mwili wa hayati Benjamin Mkapa kisha mwili wake kupelekwa kijijini kwao Lupaso kwa ajili ya maziko Jumatano ya tarehe 29 Julai.