Jumamosi , 28th Feb , 2015

Wanawake nchini Tanzania wametakiwa kutopuuzia mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye mfumo wao wa uzazi kwani zinaweza kuwa dalili za ugonjwa hatari wa saratani ya shingo ya kizazi.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo – WAMA ambaye ni mke wa Rais mama Salma Kikwete, ametoa angalizo hilo leo jijini Dar es Salaam, wakati akikabidhi mashine mpya ya kupima ugonjwa wa saratani kwa hospitali ya jeshi Lugalo.

Kwa mujibu wa Mama Kikwete, suala la kubaini dalili hatarishi liende sambamba na wanawake hao kujenga tabia ya kwenda mara kwa mara katika vituo vya afya, kupima ili kubaini iwapo wana matatizo ya saratani ili wapate matibabu mapema.

Aidha mama Kikwete amewataka wagonjwa na jamii nzima pindi wagundulikapo wana maambukizi ya maradhi hayo wasikate tamaa na kujiona kama hawana uwezo tena wakufanya kazi zakuwasaidia kimaisha na kusubiri kufa.

Wakati huohuo mnadhimu mkuu wa jeshi la wananchi wa Tanzania Mnadhimu mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Samweli Ndomba amesema kuwa mashine hizo zitafanya kazi kwa kila mwananchi wa Tanzania bila kubagua raia na askari.

Mganga mkuu wa Hospital hiyo ya Lugalo Brigedia Josia Makele amesema kuwa idadi kubwa ya wananchi wanaofika hospital hapo kupata matibabu ni wagonjwa ambao ugonjwa umefikia hatua mbaya hivyo kuwalazimu kuwasaidia kimatibabu kwanza bila kubagua.