Jumapili , 3rd Dec , 2017

Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewaomba wazazi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wahakikishe wanatumia sehemu ya kipato chao katika kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao ikiwa ndio njia pekee inayoweza kumsaidia mtoto katika kutimiza ndoto zake

Mama Mary amesema hayo katika mahafali ya shule ya awali na msingi ya Wonder Kids, iliyopo wilayani Ruangwa, Lindi ambapo alialikwa katika mahafali hayo kama mdau wa elimu.

Mama Mary ameongeza kuwa Walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanafunzi hao wanajua kusoma vizuri, hivyo wazazi watumie kipato chao kuwekeza katika elimu kwani faida watakuja kuiona baadaye.

Pia Mama Mary ametumia fursa hiyo kuwaomba wazazi wawatie moyo walimu kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa hivyo wazazi washiriki kikamilifu katika suala la elimu kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya masomo yao badala ya kuwaachia walimu peke yao.